TAMKO LA PAMOJA LA FUNGAMANO
LA MAKANISA YA KILUTHERI DUNIANI NA LA KANISA
KATOLIKI JUU YA MAFUNDISHO YA KUHESABIWA HAKI

 

UTANGULIZI 

1. Mafundisho juu ya kuhesabiwa haki yalikuwa na umuhimu wa msingi kwa Matengenezo ya Kilutheri ya karne ya kumi na sita. [Mafundisho] hayo yalifikiriwa kuwa “fungu la kwanza na la msingi” [1], na wakati huohuo [mafundisho] “yanayosimamia na kuamulia mafundisho mengine yote ya kikristo” [2]. Mafundisho ya kuhesabiwa haki yalishikiliwa na kutetewa sana, katika maana yake kadiri ya Matengenezo na katika uzito wake wa pekee, mbele ya Kanisa Katoliki la Kiroma na ya theolojia vya wakati ule, ambavyo,kwa upande wake, vilikuwa vikishikilia na kutetea mafundisho ya kuhesabiwa haki yenye mwono tofauti. Kadiri ya mtazamo wa Matengenezo, kuhesabiwa haki kulikuwa kiini cha mabishano yote. Kiri za kilutheri [3]na Mtaguso Mkuu wa Trento wa Kanisa Katoliki vilitoa laana za kimafundishozinazodumu mpaka sasa na kuwa na athari ya utengano baina ya makanisa.

2. Mafundisho ya kuhesabiwa haki yameendelea kushika umuhimu huu wa pekee katika mapokeo ya kilutheri. Ndiyo sababu tangu mwanzo yamekuwa na nafasi kubwa katika dialogia rasmi ya kilutheri-kikatoliki pia.

3. Tukumbuke hasa ripoti zifuatazo: “Injili na Kanisa” (1972) [4] na “Kanisa na kuhesabiwa haki” (1994) [5] za Tume ya pamoja ya kilutheri-kikatoliki; tena, ripoti “Kuhesabiwa haki kwa imani” (1983) [6] ya dialogia ya kilutheri-kikatoliki ya Marekani; na “Laana [za kimafundisho] za wakati wa Matengenezo bado zinatenganisha [Makanisa]?” (1986) [7] ya warsha ya kiekumeni ya Wanatheolojia Waprotestanti na Wakatoliki katika Ujerumani. Baadhi ya hati hizo za dialogia zimepokelewa rasmi na Makanisa. Mfano muhimu wa mapokezi hayo ni jawabu lenye mamlaka kuhusu uchunguzi, “Laana...”, lililotolewa na Kanisa la Muungano la Kiinjili la Kilutheri la Ujerumani, pamoja na makanisa mengine ya Kanisa la Kiinjili katika Ujerumani, mwaka 1994. Hati hiyo imetambuliwa rasmi kikanisa kwa kiwango cha juu kabisa [8].

4. Katika mijadala yake juu ya mafundisho ya kuhesabiwa haki, ripoti zote za dialogia, pamoja na majibu [yanayohusiana nazo], zinaonyesha kiwango kikubwacha maafikiano katika mitazamo na katika mahitimisho. Kwa hiyo, umefika wakati wa kutathmini matokeo ya mazungumzo juu ya kuhesabiwa haki na kuyafanyia muhtasari ili makanisa yetu yapate taarifa ya matokeo ya jumla ya mazungumzo hayo, kwa usahihi na kwa ufupi kama ipasavyo, na hivyo yawezeshwe kufanya maamuzi yenye mamlaka.

5. Hili ndilo lengo la Tamko la pamoja: yaani kuonyesha kwamba Makanisa ya Kilutheri na Kanisa Katoliki [9] yenye kutia sahihi, yanaweza sasa kutamka, juu ya msingi wa mazungumzo yao, ufahamu wa pamoja wa kuhesabiwa haki kwetu, [tulikotendewa] na neema ya Mungu kwa njia ya imani katika Kristo. [Tamko hili] halina mambo yote ambayo kila Kanisa linafundisha juu ya kuhesabiwa haki; [lakini] linadhihirisha maafikiano juu ya kweli kadhaa za msingi za mafundisho ya kuhesabiwa haki, na kuonyesha kwamba tofauti zinazobaki katika ufafanuzi wake zimekoma kuwa na athari ya kusababisha laana za kimafundisho.

6. Tamko letu si kauli mpya inayojitegemea, isiyohusiana na ripoti za mazungumzo na hati zilizolitangulia; wala halichukui nafasi ya hizo. Bali [tamko hilo] lina marejeo mengi ya hati hizo na ya hoja zake, kama kiambatisho juu ya machimbuko kinavyoonyesha.

7. Kama vile mazungumzo yenyewe, kadhalika tamko hili la pamoja, msimamo wake ni kwamba katika kutatua masuala yenye matata na kufuta laana za kimafundisho vya zamani, makanisa hayahesabu hizo laana kama mambo hafifu, wala hayakani historia zake za nyuma. Kinyume chake, tamko hilo limetoka katika imani kwamba Makanisa yetu, katika historia zake maalum, yamekuwa yakipata utambuzi mpya. Imejitokeza michakato ambayo haiwezeshi tu, bali inadai pia Makanisa yachambue na kuwa na mtazamo mpya juu ya masuala yaliyoleta utengano na juu ya laana [za kimafundisho].

 

1. UJUMBE WA BIBLIA JUU YA KUHESABIWA HAKI

8. Njia yetu ya pamoja ya kusikia Neno la Mungu katika Maandiko Matakatifu, imetuelekeza katika utambuzi huo mpya. Twasikia kwa pamoja Injili [itangazayo] kwamba “Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yn 3:16). Habari njema hiyo yatangazwa katika Maandiko Matakatifu kwa namna mbalimbali. Katika Agano la Kale twasikia Neno la Mungu kuhusu dhambi ya wanadamu (Zab 51:1-5; Dn 9:5 nk; Mhu 8:10 nk; Eze 9:16 nk) na uasi wa wanadamu (Mwa 3:1-19; Neh 9:16-17.26), pamoja na “haki” ya Mungu (Isa 46:13;51:5-8;56:1;53:11; Yer 9:24) na “hukumu” yake (Mhu 12:14; Zab 9:4 nk;76:8-10).

9. Katika Agano Jipya, namna mbalimbali za kueleza “haki” na “kuhesabiwa haki” zinapatikana katika Injili ya Mathayo (5:10;6:33;21:32) na ya Yohane (16:8-11), katika waraka kwa Waebrania (5:1-3;10:37), na katika waraka wa Yakobo (2:14-26)[10]. Pia katika nyaraka za mtume Paulo, kipawa cha wokovu huelezwa kwa semi mbalimbali, zikiwamo, “Kristo ametuweka huru kwa ajili ya uhuru” (Gal 5:1-13; taz. Rum 6:7), “Kupatanishwa na Mungu” (“ Kor 5:18-21; taz. Rum 5:11), “Kuwa na amani kwa Mungu” (Rum 5:1), “Kuwa kiumbe kipya” (2 Kor 5:17), “Kuwa hai kwa Mungu katika Kristo Yesu” (Rum 6:11.23), tena “Kutakaswa katika Kristo Yesu” (taz. 1Kor 1:2.30; 2Kor 1:1). Miongoni mwa semi hizo, [ule uelezao kuwa] wanadamu wenye dhambi “huhesabiwa haki kwa neema ya Mungu kwa njia ya imani” (Rum 3:23-25), una nafasi kuu. Huo ndio uliopewa umuhimu wa pekee wakati wa Matengenezo.

10. [Mtume] Paulo hutaja Injili kama uweza wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa mtu aliyeanguka chini ya utawala wa dhambi; tena kama habari itangazayo kwamba “Haki ya Mungu imedhihirishwa toka imani hata imani” (Rum 1:17 nk), na kuleta “kuhesabiwa haki” (Rum 3:13-21). Naye [Paulo] amhubiri Kristo kama “Haki yetu” (1Kor 1:30), kwa kulihusisha na Bwana mfufuka lile alilolitangaza [nabii] Yeremia kwa habari ya Mungu mwenyewe (Yer 23:6). Katika kifo na ufufuko wa Kristo, mambo yote ya tendo lake la wokovu yana mizizi yake, kwa maana Yeye ni Bwana wetu “ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu na kufufuliwa ili tupate kuhesabiwa haki”(Rum 4:25). Wanadamu wote wanahitaji haki ya Mungu, kwa sababu “Wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Rum 3:23; taz. Rum 1:18; 3:20; 11:32; Gal 3:22). Katika waraka kwa Wagalatia (3:6) na katika waraka kwa Warumi (4:3-9), Paulo hutambua imani ya Ibrahimu (Mwa 15:6) kama imani kwa Mungu anayemhesabia haki mwenye dhambi; na hutaja ushuhuda wa Agano la Kale ili kutamka kwa ujasiri Injili yake, ya kwamba haki hiyo itahesabiwa kwa ajili ya wote ambao, sawasawa na Ibrahimu, wanaitumainia ahadi ya Mungu. “Mwenye haki ataishi kwa imani yake” (Hab 2:4; taz. Gal 3:11; Rum 1:17). Katika nyaraka za [Mtume] Paulo, haki ya Mungu ni pia “uweza wa Mungu kwa ajili ya kila aaminiye” (Rum 1:16-17). Katika Kristo, [Mungu] hufanya [haki yake] iwe haki yao (2Kor 5:21). Twapata kuhesabiwa haki kwa njia ya Yesu Kristo, “ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake”. (Rum 3:25; taz. 3:21-28). “Kwa maana mmeokolewa kwa neema kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo” (Efe 2:8-9).

11. Kuhesabiwa haki ni msamaha wa dhambi (Rum 3:23-25; Mdo 13:39; Lk 18:14), ukombozi kutoka katika utawala wa dhambi na wa mauti (Rum 5:12-21) na kutoka katika laana ya sheria (Gal 3:10-14). Tena ni kukaribishwa katika ushirika na Mungu; tangu sasa, ingawa hilo litakuwa kamili katika ufalme wa Mungu ujao (Rum 5:1-2). [Kuhesabiwa haki] kwaunganisha na Kristo, tena na kifo na ufufuko wake (Rum 6:5); nako kunatokea kwa kumpokea Roho Mtakatifu katika ubatizo na kwa kuingizwa katika mwili ulio mmoja (Rum 8:1-2,9-11; 1Kor 12:12-13). Na hayo yote yanatoka kwa Mungu tu, kwa ajili ya Kristo, kwa neema, kwa njia ya imani katika “Injili ya Mwana wa Mungu” (Rum 1:1-3).

12. Waliohesabiwa haki wanaishi kwa imani ambayo chanzo chake ni Neno la Kristo (Rum 10:17) na ambayo yatenda kazi kwa upendo (Gal 5:6), ulio tunda la Roho (Gal 5:22). Lakini, kwa vile Waliohesabiwa haki wazidivyo kushambuliwa ndani na nje na enzi na tamaa mbalimbali (Rum 8:35-39; Gal 5:16-21), na kuanguka katika dhambi (1Yoh 1:8-10), hawana budi sikuzote kusikia tena ahadi za Mungu, kuungama dhambi zao (1Yoh 1:9), kushiriki mwili na damu vya Kristo na kuonywa kuishi kwa haki kulingana na mapenzi ya Mungu. Ndiyo sababu Mtume [Paulo] huwaambia waliohesabiwa haki, “Utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kwa kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Flp 2:12-13). Lakini habari njema yadumu, “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu”(Rum 8:1); hao ambao Kristo yu hai ndani yao (Taz. Gal 2:20). “Kwa tendo moja la haki - la Kristo - watu wote walihesabiwa haki yenye uzima” (Rum 5:18).

 

2. MAFUNDISHO YA KUHESABIWA HAKI KAMA SUALA LA KIEKUMENI

13. Namna zenye kupingana za ufasili na za utekelezaji wa ujumbe wa Biblia juu ya kuhesabiwa haki zilikuwa kati ya sababu za msingi za utengano katika Kanisa la Magharibi katika karne ya kumi na sita, kama vile zilivyokuwa na athari kuhusu laana za kimafundisho. Ndiyo sababu ufahamu wa pamoja wa kuhesabiwa haki ni jambo la msingi na la lazima ili kushinda utengano ule. Dialogia ya kiekumeni iliyofuata Mtaguso mkuu wa Vatikano II, huku ikishika utambuzi uliotoka kwa kazi mpya za uchunguzi wa kibiblia na kutumia kazi za kisasa za utafiti wa historia ya theolojia na ya dogma[11], imeuelekezea ulinganifu muhimu kuhusu [mafundisho ya] kuhesabiwa haki. Matokeo ya ulinganifu huo ni kwamba tamko hili la pamoja linaweza kutamka maafikiano juu ya kweli kadhaa za msingi kuhusu mafundisho ya kuhesabiwa haki. Katika mwanga wa maafikiano hayo, laana za kimafundisho za karne ya kumi na sita zilizohusiana [na mafundisho ya kuhesabiwa haki], haziliathiri [Kanisa] mshirika la wakati wa sasa.

 

3. UFAHAMU WA PAMOJA WA KUHESABIWA HAKI

14. Makanisa ya Kilutheri na Kanisa Katoliki la Kiroma yamekuwa yakisikia kwa pamoja habari njema zilizotangazwa katika Maandiko Matakatifu. Kusikia huko kwa pamoja, pamoja na mazungumzo ya kitheolojia ya miaka hii ya mwisho, kumeleta ufahamu shirika wa kuhesabiwa haki, wenye maafikiano juu ya kweli za msingi. Fafanuzi zenye kutofautiana zinazopatikana katika kauli maalum mbalimbali, hazipingani na [maafikiano] hayo.

15. Katika imani, twasadiki kwa pamoja kwamba kuhesabiwa haki ni kazi ya Mungu aliye Mmoja katika Nafsi tatu. Baba amemtuma Mwanae ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Umwilisho, kifo na ufufuko wa Kristo ni msingi na asili ya kuhesabiwa haki. Kwa hiyo, maana ya kuhesabiwa haki ndiyo hii: Kristo mwenyewe ni haki yetu, ambayo twaishiriki kwa njia ya Roho Mtakatifu, kulingana na mapenzi ya Baba. Kwa pamoja twakiri: kwa neema tu, katika imani kwa tendo la wokovu la Kristo, wala si kutokana na stahili yetu yoyote, tunakubaliwa na Mungu na kupewa Roho Mtakatifu, anayefanya upya mioyo yetu na kututayarisha na kutuita kwa ajili ya matendo mema [12].

16. Watu wote wanaitwa na Mungu kupata wokovu katika Kristo. Tunahesabiwa haki kwa njia ya Kristo tu, tukipokea wokovu huo katika imani. Imani yenyewe ni kipawa cha Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu, atendaye kazi kwa njia ya Neno na ya Sakramenti katika jumuiya ya waamini, na wakati huohuo huwaongoza kwa upyaisho ule wa maisha ambao Mungu ataukamilisha katika uzima wa milele.

17. Twashiriki pia imani kwamba ujumbe wa kuhesabiwa haki hutuelekeza, kwa namna ya pekee, kwenye kiini cha ushuhuda wa Agano Jipya juu ya tendo la Mungu la wokovu katika Kristo. [Ushuhuda huo] unatutangazia kwamba sisi, huku tukiwa wenye dhambi, maisha yetu mapya yanaitegemea tu huruma ya Mungu yenye kusamehe na yenye kufanya upya, ambayo Yeye atujalia kama kipawa, nasi twaipokea katika imani, bila kuweza kuistahili kwa namna yoyote.

18. Kwa hiyo mafundisho ya kuhesabiwa haki, yapokeayo na kufafanua ujumbe huo, si tu sehemu fulani ya mafundisho ya kikristo, bali yana uhusiano wa msingi na kweli zote za imani, ambazo hatuna budi kufikiria zihusiane kiundani zenyewe kwa zenyewe. [Mafundisho ya kuhesabiwa haki] ni kigezo cha lazima kinachofaa daima ili kumwelekezea Kristo ufundishaji wote na utendaji wote wa Makanisa yetu. Walutheri, wanapotilia mkazo umuhimu wa pekee wa kigezo hicho, hawakani umuhimu wa kweli zote za imani, wala kwamba zinahusiana. Wakatoliki, wakijifikiria wamefungamana na vigezo mbalimbali, hawakani dhima maalum ya ujumbe wa kuhesabiwa haki. Walutheri na Wakatoliki wanashiriki kwa pamoja lengo la kumkiri Kristo katika mambo yote, Yeye anayetakiwa kuaminiwa juu ya mambo yote kama Mpatanishi pekee (1 Tim 2:5-6), ambaye kwa njia yake, Mungu, katika Roho Mtakatifu, ajitoa nafsi yake na kumimina vipawa vyake vyenye kufanya upya [vitu vyote]. (Taz. Machimbuko, kifungu 3).

 

4. MAELEZO YA UFAHAMU WA PAMOJA WA KUHESABIWA HAKI

4.1 UDHAIFU WA BINADAMU NA DHAMBI, KUHUSIANA NA KUHESABIWA HAKI

19. Twakiri kwa pamoja kwamba wanadamu wote wanahitaji kabisa neema ya Mungu yenye kuleta wokovu, kwa ajili ya wokovu wao. Uhuru walio nao kuhusiana na watu na vitu vya dunia hii, si uhuru kuhusiana na wokovu. Maana [wanadamu], kwa kuwa ni wenye dhambi, wapo chini ya hukumu ya Mungu, nao hawawezi kumgeukia Mungu kwa nguvu zao wenyewe kutafuta ukombozi, wala kustahili kuhesabiwa haki mbele za Mungu, wala kupata wokovu kwa njia ya uwezo wao wenyewe. Kuhesabiwa haki kunapatikana tu kwa neema ya Mungu. Kutokana na Wakatoliki na Walutheri kukiri hayo kwa pamoja, ni sahihi kusema kwamba:

20. Wakatoliki wanaposema ya kuwa wanadamu “wanashirikiana”, katika kujiandaa na kukubali kuhesabiwa haki, kwa kuridhia tendo la Mungu lenye kuhesabu haki, wanafikiria ridhaa hiyo ya mtu binafsi, si kama tendo litokalo kwa uwezo wa asili wa binadamu, bali ridhaa yenyewe kama matokeo ya neema [ya Mungu].

21. Kadiri ya fundisho la kilutheri, binadamu hawana uwezo wa kushirikiana katika kupata wokovu wao; kwa sababu, kwa vile ni wenye dhambi, wao wenyewe wampinga Mungu na tendo lake la wokovu. Walutheri hawakani kwamba mtu anaweza kukataa kazi ya neema. Wanapotilia mkazo kwamba mtu huweza kupokea tu (“mere passive”) kuhesabiwa haki, kwa njia hiyo wanataka kukana kila uwezekano wa mtu kutoa mchango kwa ajili ya kuhesabiwa haki kwake mwenyewe. Lakini hawakani kwamba waamini huhusika kikamilifu na kibinafsi katika kuamini kwao, ambako kunatoka katika Neno la Mungu. (taz. Machimbuko kifungu 4.1)

 

4.2 KUHESABIWA HAKI KAMA MSAMAHA WA DHAMBI NA KUWAFANYA WATU WENYE HAKI

22. Twakiri kwa pamoja kwamba Mungu husamehe dhambi kwa neema, na wakati huohuo huwaokoa binadamu na mamlaka ya dhambi yenye kuwatia utumwani, na kuwajalia kipawa cha maisha mapya katika Kristo. Watu wanapopata kumshiriki Kristo kwa imani, Mungu hawahesabii tena dhambi yao, na kwa njia ya Roho Mtakatifu anazalisha pendo tendaji ndani yao. Hali hizo mbili za tendo la neema la Mungu, inabidi zisitenganishwe, kwa sababu ya wanadamu kuunganishwa kwa imani na Kristo, aliye, katika nafsi yake, haki yetu (1Kor 1:30): yaani, msamaha wa dhambi, na uwepo wa Mungu mwenyewe uletao wokovu. Kwa vile Wakatoliki na Walutheri wanakiri jambo hilo kwa pamoja, ni sahihi kusema kwamba:

23. Walutheri wanapotilia mkazo kuwa haki ya Kristo ndiyo haki yetu, kusudi lao hasa ni kusisitiza kwamba mwenye dhambi anajaliwa haki mbele ya Mungu katika Kristo kwa njia ya kutangaziwa msamaha, na kwamba maisha ya mtu yanakuwa mapya katika umoja na Kristo tu. Tena, [Walutheri] wanapotilia mkazo kwamba neema ya Mungu ni upendo wenye kusamehe (“Fadhili ya Bwana” [13]), hawakani upyaisho wa maisha ya Mkristo, bali wanataka kusema kwamba kuhesabiwa haki hakufungwi na ushirikiano wa binadamu, wala hakuyategemei hata matokeo ya neema katika binadamu, ya kufanya upya maisha yao.

24. Wakatoliki, wanapotilia mkazo upyaisho wa utu wa ndani kwa njia ya kupokea neema, iliyotolewa kama kipawa kwa waamini [14], wanapenda kusisitiza kwamba neema ya Mungu yenye kusamehe huleta daima pamoja nayo kipawa cha maisha mapya, ambayo katika Roho Mtakatifu hutenda kazi katika upendo hai. Lakini hawakani kwamba kipawa cha Mungu cha neema katika kuhesabiwa haki hakiutegemei ushirikiano wa binadamu. (Taz. Machimbuko, kifungu 4.2)

 

4.3 KUHESABIWA HAKI KWA IMANI NA KWA NJIA YA NEEMA

25. Twakiri kwa pamoja kwamba wenye dhambi wanahesabiwa haki kwa imani katika tendo la Mungu la wokovu katika Kristo. Kwa tendo la Roho Mtakatifu katika ubatizo, wanajaliwa kipawa cha wokovu, kinachoweka msingi wa maisha yote ya kikristo. Nao huitegemea ahadi ya Mungu yenye fadhili, kwa imani yenye kuhesabu haki iliyo pamoja na kumtumaini Mungu na kumpenda. Imani hiyo ni hai katika upendo; ndiyo sababu Mkristo hawezi wala hapaswi kutotenda kazi. Lakini, yote yanayotangulia au kufuata kipawa huru cha imani katika mtu aliyehesabiwa haki, si msingi wa kuhesabiwa haki, wala hayawezi kudai kukustahili.

26. Kadiri ya ufahamu wa kilutheri, Mungu awahesabia haki wenye dhambi katika imani tu (sola fide). Katika imani, hao wamtegemea kikamilifu Muumba na Mkombozi wao; na hivyo wanakaa katika ushirika naye. Mungu mwenyewe anazalisha imani kwa kuamsha kumtegemea huko kwa njia ya neno lake umbaji. Tendo la Mungu ni “kuumba upya”, kwa hiyo linaathiri hali zote za binadamu na kuongoza kuishi katika matumaini na mapendo. Mafundisho ya “Kuhesabiwa haki kwa imani tu” yanatofautisha lakini hayatenganishi kuhesabiwa haki kwenyewe na upyaisho wa mwenendo wa maisha ya mtu, ambao, kwa lazima, unatokana na kuhesabiwa haki, tena ambao, pasipo huo, imani haipo. Kwa namna hii, msingi ambao upyaisho wa maisha unatokana nao, ni wazi; maana huo unatoka katika upendo wa Mungu, unaotolewa kwa ajili ya binadamu katika kuhesabiwa haki. Kuhesabiwa haki na upyaisho [wa maisha] vimeunganika katika Kristo, aliyepo katika imani.

27. Ufahamu wa kikatoliki pia unafikiria kwamba imani ni ya msingi katika kuhesabiwa haki. Maana, pasipo imani, hakuna kuhesabiwa haki . Wanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya ubatizo, kama wasikilizaji na waamini wa Neno. Kuhesabiwa haki kwa wenye dhambi ni msamaha wa dhambi na kufanywa wenye haki kwa neema yenye kuhesabu haki, itufanyayo watoto wa Mungu. Katika kuhesabiwa haki, watu waliohesabiwa haki wanapewa na Kristo imani, matumaini na mapendo, na hivyo wanakaribishwa kwenye ushirika naye [15]. Uhusiano mpya huo wa mtu binafsi na Mungu unawekwa kabisa juu ya msingi wa rehema ya Mungu, na kuzidi kutegemea sikuzote kazi yenye kuokoa na kuumba aitendayo Mungu mwenye rehema, adumuye kuwa mwaminifu kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe kusudi mtu aweze kumtumainia. Hivyo, neema yenye kuhesabu haki haitakuwa kamwe mali ya kibinadamu ambayo kwa njia yake mtu akate rufaa dhidi ya Mungu. Mafundisho ya kikatoliki yanapotilia mkazo upyaisho wa maisha kwa neema yenye kuhesabu haki, upyaisho huo katika imani, matumaini na mapendo huitegemea daima neema ya Mungu isiyochunguzika, wala hauleti mchango wowote kwa ajili ya kuhesabiwa haki, ambao kwao mtu aweze kujisifu mbele ya Mungu (Rum 3:27). (taz. Machimbuko, kifungu 4.3).

 

4.4 ALIYEHESABIWA HAKI KAMA MTU MKOSEFU

28. Twakiri kwa pamoja kwamba katika ubatizo Roho Mtakatifu amwunganisha mtu na Kristo, amhesabia haki, na kumfanya upya kwelikweli. Lakini waliohesabiwa haki wapaswa sikuzote, kwa maisha yao yote, kuitegemea neema yenye kuhesabu haki, isiyo na masharti. Nao daima hukabiliwa na uwezo wa dhambi inayowashambulia bado (taz. Rum 6:12-14), wala hawawezi kuepukana na mapambano ya maisha yote dhidi ya kumpinga Mungu kunakotokana na tamaa za ubinafsi za Adamu wa kale (taz. Gal 5:16; Rum 7:7-10). Tena, waliohesabiwa haki wapaswa kila siku kumwomba Mungu awasamehe, kulingana na “Sala ya Bwana” (Mt 6:12; 1Yoh 1:19); nao waitwa sikuzote kuongoka na kutubu, na hujaliwa sikuzote msamaha [wa dhambi].

29. Walutheri hufafanua hali hiyo ya Mkristo [kwa kutamka] kwamba yeye ni “kwa wakati mmoja mwenye haki na mwenye dhambi”. Waamini ni wenye haki kabisa, kwa maana Mungu awasamehe dhambi zao kwa njia ya Neno na ya Sakramenti, na kuwajalia haki ya Kristo, wanayojitwalia [kama haki yao] katika imani. Katika Kristo, wanafanywa wenye haki mbele ya Mungu. Lakini, kwa kujitazama nafsi zao kwa njia ya sheria, watambua kwamba wanadumu pia kuwa wenye dhambi kabisa. Dhambi yakaa bado ndani yao (1Yoh 1:8; Rum 7:17-20); maana waigeukia tena na tena miungu ya uongo, wala hawampendi Mungu kwa upendo ule usiotenganika unaodaiwa naye, kwa sababu ni Muumba wao (Kum 6:5; Mt 22:36-40). Kumpinga Mungu huko, kwa namna hiyo, ni dhambi kweli. Lakini, mamlaka ya dhambi yenye kutia utumwani imevunjwa kwa njia ya stahili ya Kristo. Si tena dhambi “inayomtawala” Mkristo, kwa maana [dhambi] yenyewe “imetawaliwa” na Kristo, ambaye waliohesabiwa haki wameunganika naye katika imani. Kwa hiyo, basi, Wakristo, katika maisha ya sasa, waweza kwa kiasi fulani kuishi maisha ya haki. Licha ya dhambi, Mkristo si tena katika hali ya utengano na Mungu; maana, kwa kuurudia ubatizo kila siku, mtu aliyezaliwa upya kwa ubatizo na Roho Mtakatifu hupata kusamehewa dhambi yake ile. Hivyo, dhambi hiyo haileti tena laana na mauti ya milele [16]. Kwa hiyo, Walutheri, wanaposema kwamba watu waliohesabiwa haki ni wenye dhambi pia, tena kwamba kumpinga Mungu kwao, kwa kweli ni dhambi, hawakani kwamba, licha ya dhambi, hawatengani na Mungu wala hawakani kwamba dhambi hiyo ni dhambi “iliyotawaliwa”. Licha ya tofauti zilizomo katikakufafanua “dhambi katika waliohesabiwa haki”, [Walutheri] wanapatana na Wakatoliki katika kauli hizo.

30. Wakatoliki hushikilia kwamba neema ya Yesu Kristo iliyotolewa katika ubatizo, huyaondoa yote yaliyo dhambi “kwa maana yake halisi” (in the proper sense) na “kustahili hukumu ya adhabu” (Rum 8:1) [17]; isipokuwa mwelekeo (tamaa) utokao katika dhambi na kusukuma kwa dhambi, hudumu ndani ya binadamu. Lakini, Wakatoliki hawaoni mwelekeo huo kama dhambi, kadiri ya maana yake halisi. Maana, kulingana na msimamo wa kikatoliki, dhambi ya binadamu inahitaji daima mchango wa mtu binafsi (a personal element); lakini mwelekeo huo [peke yake] unapungukiwa na mchango huo. Hata hivyo, Wakatoliki hawakani kwamba mwelekeo huo haupatani na mpango wa asili wa Mungu kwa ajili ya wanadamu, tena kwamba kihalisi mwelekeo huo unapingana na Mungu na kuendelea kuwa adui wa mtu katika mapambano yake ya maisha yote. Lakini [Wakatoliki], wakiwa na moyo wa shukrani kwa ukombozi [waliopata] kwa Kristo, wanasisitiza kwamba mwelekeo huo unaompinga Mungu haustahili adhabu ya mauti ya milele [18], wala haumtenganishi mtu aliyehesabiwa haki na Mungu. Lakini watu, wanapojitenga kwa makusudi na Mungu, kurudi kwao kuzishika tena amri hakutoshi, bali lazima wapokee msamaha na amani katika Sakramenti ya Upatanisho kwa njia ya neno la msamaha wajaliwalo kwa kazi ya Mungu ya kupatanisha katika Kristo. (taz. Machimbuko, kifungu 4:4)

 

4.5 SHERIA NA INJILI

31. Twakiri kwa pamoja kwamba wanadamu wanahesabiwa haki kwa imani katika Injili “pasipo matendo ya sheria” (Rum 3:28). Kristo ameitimiliza sheria, na kwa kifo na ufufuko wake, ameidhoofisha kama njia ya kupata wokovu. Twakiri pia kwamba amri za Mungu zinaendelea kuwa na uhalali wake kwa waliohesabiwa haki, na kwamba Kristo, kwa njia ya mafundisho yake na mfano wake, amedhihirisha mapenzi ya Mungu, ambayo ni kanuni kwa ajili ya mwenendo wa waliohesabiwa haki pia.

32. Walutheri wanasisitiza kwamba kutofautisha sheria na Injili na kuzipanga kwa usahihi kulingana na viwango vyake, ni muhimu sana kwa ajili ya ufahamu wa kuhesabiwa haki. Sheria, katika matumizi yake ya kitheolojia, ni kudai na kushutumu. Wakati wa maisha yao, watu wote, hata Wakristo, kwa sababu ni wenye dhambi, wawekwa chini ya kushutumu huko kunakofunua dhambi yao, ili, katika imani kwa Injili, waigeukie kikamilifu huruma ya Mungu katika Kristo, ambayo yenyewe tu yawahesabia haki.

33. Sheria kama njia ya wokovu imetimilizwa na kudhoofishwa kwa njia ya Injili; ndiyo sababu Wakatoliki waweza kusema kwamba Kristo si mtoaji sheria kwa mfano wa Musa. Wakatoliki, wanapotilia mkazo kwamba waliohesabiwa haki lazima wazishike amri za Mungu, hawakani kwamba kwa njia ya Yesu Kristo Mungu amewaahidia kwa huruma watoto wake neema ya uzima wa milele [19]. (taz. Machimbuko, kifungu 4.5)

 

4.6 UHAKIKISHO WA WOKOVU

34. Twakiri kwa pamoja kwamba Waamini waweza kutegemea huruma ya Mungu na ahadi zake. Licha ya udhaifu wao na matishio mbalimbali kwa imani yao, waweza kuitegemea, juu ya msingi wa nguvu ya kifo cha Kristo na ufufuko wake, ahadi yenye kuleta matokeo ya neema ya Mungu katika Neno na katika Sakramenti, na hivyo kuwa na hakika ya neema hiyo.

35. Mababa wa Matengenezo walitilia mkazo suala hilo kwa namna ya pekee: katika majaribu, waamini hawapaswi kutegemea nafsi zao, bali humtegemea Kristo tu, na kumtumaini Yeye peke yake. Nao, wakiitumainia ahadi ya Mungu, wanahakikishiwa kuhusu wokovu wao; lakini, kamwe hawatakuwa na uhakika [wa wokovu huo], kama wakijitazama wenyewe.

36. Wakatoliki wanaweza kushiriki msimamo wa Mababa wa Matengenezowa kuiweka imani juu ya msingi wa uhalisi wa ahadi ya Kristo, bila kufikiria mang’amuzi ya mtu binafsi; tena [kushiriki] msimamo wa kulitumainia tu Neno la Kristo lenye kusamehe (taz. Mt 16:19; 18:18). Kufuatana na Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, Wakatoliki wamesisitiza kwamba kuwa na imani ni kujikabidhi kikamilifu kwa Mungu [20], anayetuokoa kutoka katika giza la dhambi na la mauti na kutufufua kwa uzima wa milele [21]. Kutokana na hilo, mtu hawezi kumwamini Mungu na wakati huohuo kufikiria ahadi ya Mungu kama isiyoaminika. Hapana mtu awezaye kuwa na shaka juu ya huruma ya Mungu na stahili ya Kristo; ingawa inawezekana kila mtu awe na wasiwasi juu ya wokovu wake anapotazama unyonge wake na kasoro zake. Lakini, anapotambua kushindwa kwake, hata hivyo mwaamini aweza kuwa na hakika kwamba Mungu anataka wokovu wake.

 

4.7 MATENDO MEMA YA MTU ALIYEHESABIWA HAKI

37. Twakiri kwa pamoja kwamba matendo mema - yaani kuishi maisha ya kikristo katika imani, matumaini na mapendo - yatoka kwa kuhesabiwa haki, tena ni matunda yake. Waliohesabiwa haki, wanapoishi katika Kristo na kutenda katika neema waliyojaliwa, wanazaa – kadiri ya usemi wa kibiblia – matunda mazuri. Wakati huohuo, kutokana na Wakristo kupambana na dhambi kwa maisha yao yote, matokeo hayo ya kuhesabiwa haki ni wajibu ambao lazima wautimize. Ndiyo sababu Yesu, pamoja na maandishi ya Mitume, huwaonya Wakristo watoe matunda ya matendo ya upendo.

38. Kadiri ya ufahamu wa kikatoliki, matendo mema, yawezekanayo kufanyika kwa neema na kwa kazi ya Roho Mtakatifu, yasaidia kukua katika neema, na hivyo haki itokayo kwa Mungu kuhifadhiwa, na ushirika na Kristo kuwa na kina zaidi. Wakatoliki, wanaposisitiza sifa ya matendo mema ya kuwa ni “yenye kustahili”, wanataka kusema kwamba thawabu inaahidiwa mbinguni kwa matendo hayo, kulingana na ushuhuda wa Biblia. Lengo lao ni kutilia mkazo uwajibikaji wa binadamu katika kutenda kwao, bila kukanusha sifa ya matendo hayo ya kuwa ni vipawa [vya Mungu], wala kamwe hawakani kwamba kuhesabiwa haki kwaendelea kuwa kipawa cha neema ambacho mtu hakistahili.

39. Dhana ya kuhifadhi neema na ya kukua katika neema na katika imani inashikiliwa na Walutheri pia. Hao wanatilia mkazo kwamba haki, kama ridhaa ya Mungu na kama ushiriki wa haki ya Kristo, daima ni timilifu. [Lakini], wakati huohuo [Walutheri] wanasisitiza kwamba inawezekana pawepo ukuaji katika matokeo yake katika maisha ya kikristo. [Walutheri], wanapofikiria matendo mema ya Wakristo kama matunda ya kuhesabiwa haki na ishara zake, wala si kama “stahili” za mtu, kwa vyovyote wanafafanua uzima wa milele, kulingana na Agano Jipya, kama “thawabu” ambayo mtu haistahili, kwa maana ya kwamba ni utimizaji wa ahadi ya Mungu kwa ajili ya waamini. (taz. Machimbuko, kifungu 4.7).

 

5. UMUHIMU NA LENGO LA MAAFIKIANOYALIYOFIKIWA

40. Ufahamu wa mafundisho ya kuhesabiwa haki uliotangazwa katika tamko hili unaonyesha kwamba pana maafikiano baina ya Walutheri na Wakatoliki juu ya kweli kadhaa za msingi za mafundisho ya kuhesabiwa haki. Kwa mwanga wa maafikiano hayo, tofauti zinazobaki za usemi, za ufafanuzi wa kitheolojia na za mkazo katika ufahamu wa kuhesabiwa haki, zilizotajwa katika aya 18-39, zinakubalika. Kwa hiyo, maelezo ya kilutheri na maelezo ya kikatoliki ya kuhesabiwa haki, hayajifungi yenyewe kwa yenyewe katika tofauti zake, wala hayaharibu maafikiano juu ya hizo kweli za msingi.

41. Kwa hiyo, laana za kimafundisho za karne ya kumi na sita, kwa kadiri zinavyohusiana na mafundisho ya kuhesabiwa haki, zinaonekana kwa mtazamo mpya. Fundisho la Makanisa ya Kilutheri lililotolewa katika tamko hili halipo chini ya laana za Mtaguso wa Trento. Laana zilizomo katika Kiri za Kilutheri hazihusu fundisho la Kanisa Katoliki la Kiroma lililotolewa katika tamko hili.

42. Hata hivyo uzito wa laana zihusianazo na mafundisho ya kuhesabiwa haki haupunguzwi. Baadhi ya [laana] hizo hazikuwa pasipo maana. Hizo zinadumu kuwa kwa ajili yetu “maonyo ya kufaa” ambayo hatuna budi kuyazingatia katika ufundishaji wetu na katika kutenda kwetu [22].

43. Maafikiano yetu juu ya kweli kadhaa za msingi za mafundisho ya kuhesabiwa haki lazima yawe na uwezo wa kuathiri maisha na ufundishaji wa Makanisa yetu, na kuthibitika katika hayo. Pana bado masuala yenye umuhimu wa viwango mbalimbali yanayohitaji kubainishwa zaidi, ikiwa ni pamoja na uhusiano wa Neno la Mungu na mafundisho ya Kanisa, eklesiolojia (elimu juu ya Kanisa), mamlaka katika Kanisa, umoja wa Kanisa, huduma, Sakramenti, uhusiano wa kuhesabiwa haki na maadili ya kijamii. Twaamini kwamba maafikiano tuliyoyapata ni msingi imara kwa ajili ya ubainifu huo. Makanisa ya Kilutheri na Kanisa Katoliki la Kiroma yataendelea kujitahidi pamoja ili ufahamu huu wa pamoja wa kuhesabiwa haki uzidi kukua na kuzaa matunda katika maisha na ufundishaji wa Makanisa .

44. Twamshukuru Bwana kwa hatua hii muhimu sana katika njia ya kushinda utengano wa Kanisa. Tumwombe Roho Mtakatifu atuongoze zaidi na zaidi kuelekea umoja ule wa kuonekana ulio mapenzi ya Kristo.

 

 

 

 

Machimbuko ya “Tamko la pamoja juu ya mafundisho ya kuhesabiwa haki”

 

Katika vifungu vya 3 na 4 vya “Tamko la pamoja”, zinarejewa fafanuzi zinazotoka katika mazungumzo mbalimbali ya kilutheri-kikatoliki, yaani katika hati hizi:

I) Kauli ya Tume ya pamoja ya kikatoliki-kilutheri juu ya Ukiri wa Augsburg, “Wote chini ya Kristo mmoja” (1980)

II) Maoni ya Kamati ya pamoja ya Kanisa la Muungano la Kiinjili la Kilutheri katika Ujerumani na ya Kamati ya kitaifa ya Ujerumani ya Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani juu ya hati “Laana za wakati wa Matengenezo, zinatenganisha bado?” (1993)

III) Denzinger-Schonmetzer, Enchiridion Symbolorum... matoleo 32-36

IV) Denzinger-Schonmetzer, Enchiridion Symbolorum... kutoka matoleo 37

V) Maoni ya Tume ya Kipapa kwa Ukuzaji wa Umoja wa Wakristo, juu ya uchunguzi, “Laana za wakati wa Matengenezo, zinatenganisha bado?” (1992)

VI) Hati “Kuhesabiwa haki kwa imani; mazungumzo baina ya Walutheri na Wakatoliki” ya Tume ya kikatoliki-kilutheri ya Marekani (1985)

VII) Hati “Laana za wakati wa Matengenezo, zinatenganisha bado?”, iliyotolewa na Karl Lehmann na Wolfhart Pannenberg (1990)

Juu ya kifungu cha 3 (aya 14-18) “Ufahamu wa pamoja wa kuhesabiwa haki”
(Taz. VII, 68-69; II,95):

- “Taswira ya kuhesabiwa haki iliyo na msingi katika imani na iliyofikiriwa kwa maana ya kisheria, ina umuhimu mkuu kwa [Mtume] Paulo na, kwa namna fulani, kwa Biblia nzima, ingawa si namna pekee ya Biblia wala ya [Mtume] Paulo ya kueleza tendo la Mungu la wokovu ” (VI, 146)

- “Wakatoliki, sawa na Walutheri, wanaweza kukiri haja yao ya kuchanganua desturi, asasi na dhana za theolojia za Kanisa, kadiri zinavyolisaidia au kuliwekea kikwazo ‘tangazo la ahadi za Mungu za hiari na zenye huruma katika Kristo Yesu, ambazo inawezekana kuzipokea vizuri kwa njia ya imani tu.” (VI:153)

 

Kuhusu “kauli ya msingi” (VI:157), inasemwa:

- “Kauli hii, kama vile mafundisho ya Matengenezo juu ya kuhesabiwa haki kwa imani tu, inafaa kama kigezo cha kutathmini mazoea, asasi na desturi vyote vya Kanisa, kwa sababu inalingana na [msemo] “Kristo tu” (solus Christus). [Kwa maana], hatimaye, Yeye tu anatakiwa kuaminiwa kama Mpatanishi pekee ambaye kwa njia yake Mungu humimina vipawa vyake vya wokovu katika Roho Mtakatifu. Sisi sote, tunaoshiriki mazungumzo haya, tunatamka kwamba mafundisho, desturi na huduma vyote vya kikristo vinatakiwa kuwa na lengo la kukuza ‘utii wa imani’ (Rum 1:5) kwa tendo la Mungu lenye kuokoa katika Kristo Yesu tu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, kwa ajili ya wokovu wa waamini na kwa ajili ya sifa na heshima ya Baba wa mbinguni" (VI,160).

- “Ndiyo maana mafundisho ya kuhesabiwa haki, na hasa msingi wake wa kibiblia, yadumu kuwa na dhima ya pekee katika Kanisa. Dhima hiyo ni sikuzote kuwakumbusha Wakristo kwamba sisi wenye dhambi twaishi kwa sababu ya upendo wa Mungu wenye kusamehe, tunaoweza tu kukubali tujaliwe, lakini hatuwezi kamwe, hata kidogo, ‘kuustahili’ wala kuubana kwa njia ya masharti yoyote, yawe yenye kutangulia au yenye kufuata [upendo huo]. Kwa hiyo mafundisho ya kuhesabiwa haki ni sikuzote kipimo ili kupambanua kama ufasili maalum mmojawapo wa uhusiano wetu na Mungu unaweza kuitwa “wa kikristo” [au hapana]. Wakati huohuo [mafundisho ya kuhesabiwa haki] ni sikuzote kipimo kwa Kanisa, ili kupambanua kama kuhubiri na kutenda kwake kunalingana na mambo aliyolijalia Bwana wake [au hapana].” (VII, 69)

- Kuafikiana kwamba mafundisho ya kuhesabiwa haki ni muhimu si tu kama fundisho mojawapo katika ufundishaji mzima wa Makanisa yetu, bali pia kama kipimo cha kupambanua mafundisho yote na utendaji wote wa Makanisa yetu, ni maendeleo ya msingi, kadiri ya mtazamo wa kilutheri, katika dialogia ya kiekumeni kati ya Makanisa yetu. Haiwezekani kufurahi kwa namna ya kutosha kwa ajili ya [maafikiano] hayo.” (II, 95; taz. 197)

- “Kwa Walutheri na Wakatoliki, mafundisho ya kuhesabiwa haki yako katika daraja tofauti katika ngazi ya Kweli za imani. Lakini pande zote mbili zinapatana kwamba mafundisho ya kuhesabiwa haki yana dhima maalum ya kuwa sikuzote kipimo ili kupambanua kama ufasili maalum mmojawapo wa uhusiano wetu na Mungu unaweza kuitwa “wa kikristo” [au hapana]. Wakati huohuo [mafundisho ya kuhesabiwa haki] ni sikuzote kipimo kwa Kanisa, ili kupambanua kama kuhubiri na kutenda kwake kunalingana na [mambo] aliyolijalia Bwana wake, [au hapana].” (VII, 69)

- “ Itabidi kuchunguza zaidi umuhimu wa mafundisho ya kuhesabiwa haki kama kigezo kwa ajili ya sakramentolojia (elimu juu ya Sakramenti), kwa ajili ya eklesiolojia (elimu juu ya Kanisa), na kwa ajili ya mafundisho ya maadili.” (V, 96)

 

Juu ya kifungu 4:1 (aya 19-21) , “Udhaifu wa binadamu na dhambi, kuhusiana na kuhesabiwa haki”
(VII, 42-26; II, 77-81; 83-84) :

- “Wale ambao ndani yao dhambi inatawala, hawawezi kufanya kitu ili kustahili kuhesabiwa haki. [Kuhesabiwa haki] ni kipawa huru cha neema ya Mungu. Hata awali za kuhesabiwa haki, kwa mfano toba, ombi kwa ajili ya [kupata] neema, na kutamani msamaha, hazina budi kuwa kazi ya Mungu ndani yetu.” (VI, 156.3)

- “Pande zote mbili [(Walutheri na Wakatoliki)] wanajitahidi kueleza wazi kwamba ... wanadamu hawawezi kuhesabu juhudi zao wenyewe kuwa zinastahili kudharauliwa. ....Lakini “itikio” ina maana tofauti na “tendo”. Itikio la imani, lenyewe linasababishwa na neno la ahadi lisiloshurutika, linalowajia wanadamu toka nje ya wao wenyewe. ‘Ushirikiano’ [wa wanadamu] unawezekana, lakini tu kwa maana ya kwamba katika imani moyo umehusika, Neno linapougusa na kuiumba imani” (VII, 46-47)

- “Lakini endapo fundisho la kilutheri likifasili uhusiano wa Mungu na wanadamu walio wake, katika kuhesabiwa haki, kwa kutilia mkazo “monoergismi” ya Mungu [(yaani Mungu tu kutenda kazi)], au Kristo tu kuleta mafanikio, kwa jinsi inayosababisha kuhesabu hiari ya mtu ya kukubali neema ya Mungu – nayo [hiari] yenyewe ni kipawa cha Mungu – kama jambo lisilo na dhima muhimu yoyote katika kuhesabiwa haki, ndipo tu kanuni 4, 5 na 9 za Mtaguso Mkuu wa Trento zitakapoendelea kuonyesha tofauti muhimu ya kimafundisho juu ya kuhesabiwa haki.” (V, 22)

- “Kwa upande wa Walutheri, kutilia mkazo katika wanadamu kutotenda kazi kuhusu kuhesabiwa haki kwao, kamwe hakukuwa na maana ya kukanusha kushiriki kwao, kikamilifu na kibinafsi, katika kuamini; bali maana yake ni kukana ushirikiano wowote katika tukio lenyewe la kuhesabiwa haki. Kuhesabiwa haki ni tendo la Kristo tu, ni tendo la neema tu.” (II, 84, 3-8)

 

Juu ya kifungu 4:2 (aya 22-24), “Kuhesabiwa haki kama msamaha wa dhambi na kuwafanya watu wenye haki”
(VI, 98-101; VII, 47 na zifuatazo; II, 84 na zifuatazo. Taz. pia madondoo ya kifungu 4.4)

- “Kwa njia ya kuhesabiwa haki, kwa wakati mmoja tunatangazwa na kufanywa wenye haki . Kwa hiyo kuhesabiwa haki si jambo linalobuniwa kisheria. Mungu, anapohesabia haki, azalisha mambo anayoahidi; asamehe dhambi na kutufanya kwa kweli wenye haki.” (VI, 156.5)

- “Theolojia ya kiprotestanti haiachi kutilia maanani jambo linalosisitizwa na mafundisho ya kikatoliki, yaani tabia ya upendo wa Mungu ya kuumba na ya kufanya upya. Wala [theolojia ya kiprotestanti] haisemi kwamba Mungu hana nguvu juu ya dhambi, kana kwamba katika kuhesabiwa haki [dhambi] imesamehewa ‘tu’, lakini haikukomeshwa kwa kweli katika uwezo wake wa kumtenganisha mwenye dhambi na Mungu”. (VII,49)

- “Mafundisho ya kilutheri hayakufikiria katu kwamba ‘kupata kuhesabiwa haki kwa njia ya Kristo’ hakuathiri maisha ya waamini. Maana neno la Kristo hutimiza mambo linayoyaahidi. Kufuatana na hilo, mafundisho ya kilutheri hutambua neema kama fadhili ya Bwana, lakini vilevile pia kama nguvu yenye kuleta matokeo.... ‘Maana panapo msamaha wa dhambi, pana pia uzima na wokovu’”. (II, 86:15-23)

- “Mafundisho ya kikatoliki hutilia maanani jambo linalosisitizwa na theolojia ya kilutheri, yaani neema kama uhusiano [wa Mungu] na mtu binafsi (the personal character of grace); tena, kwamba [neema] inahusiana na Neno. Wala [theolojia ya kikatoliki] haioni neema kama ‘mali’ halisi ya binadamu (hata kama mali aliyopewa), wala kama kitu anachoweza kukitumia kama atakavyo mwenyewe.” (VII, 49)

 

Juu ya kifungu 4:3 (aya 25-27), “Kuhesabiwa haki kwa imani na kwa njia ya neema”
(VI, 105 na zifuatazo; VII, 49-53; II, 87-90)

- “Kama tukitafsiri kutoka “lugha” moja kwenda kwa “lugha” nyingine, ndipo usemi wa kiprotestanti kuhusu kuhesabiwa haki kwa njia ya imani utakapolingana na usemi wa kikatoliki kuhusu kuhesabiwa haki kwa njia ya neema. Tena, kwa upande mwingine, mafundisho ya kiprotestanti humaanisha kimsingi kwa njia ya neno moja ‘imani’, mambo yaleyale ambayo mafundisho ya kikatoliki huyajumlisha kwa njia ya [maneno] matatu ‘imani, matumaini na mapendo’ (kulingana na 1Kor 13:13).” (VII,52)

- “Tunasisitiza kwamba imani, kulingana na amri ya kwanza, ina daima maana ya kumpenda Mungu na kumtumaini; nayo hujidhihirisha katika upendo kwa jirani.” (II,89:8-11)

- “Wakatoliki wanafundisha – sawa na Walutheri - kwamba hakuna jambo lenye kutangulia kipawa huru cha imani, linalostahili kuhesabiwa haki; tena kwamba vipawa vyote vya Mungu vyenye kuleta wokovu vyaja kwa njia ya Kristo tu.” (VI;105)

- Mababa wa Matengenezo waliona imani kama msamaha na ushirika na Kristo uliotendeka kwa neno lenyewe la ahadi. Hilo ni msingi kwa ajili ya utu mpya, ambao kwa njia yake mwili wa nyama umeifia dhambi, na mtu mpya, awe wa kiume ama wa kike, hupata uhai katika Kristo (sola fide per Christum). Lakini, ingawa kwa lazima imani hiyo humfanya upya binadamu, Mkristo aweka msingi wa kutegemea kwake si juu ya maisha yake mapya, bali tu juu ya ahadi ya Mungu yenye rehema. Kukubali katika Kristo kunatosha, kama ‘imani’ ikifahamika kama ‘kutegemea katika ahadi’ (fides promissionis). (VII,50)

- Taz. Mtaguso Mkuu wa Trento, kikao cha 6, sura ya 7, “...Kutokana na hilo, katika mchakato wa kuhesabiwa haki, mtu hupokea, pamoja na msamaha wa dhambi, [vipaji] hivi vyote anavyomiminiwa kwa wakati mmoja: imani, matumaini na mapendo, kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye katika Yeye mtu amepandikizwa”

- “Kadiri ya ufasiri wa kiprotestanti, imani inayoishikilia pasipo sharti ahadi ya Mungu katika Neno na katika Sakramenti, inatosha ili kuhesabiwa haki mbele ya Mungu; hata upyaisho wenyewe wa mtu, ambao pasipo huo hapana imani, hautoi kwa upande wake mchango wowote kwa ajili ya kuhesabiwa haki.” (VII,52)

- “Sisi Walutheri twadumu kutofautisha baina ya kuhesabiwa haki na kutakaswa, tena baina ya imani na matendo; lakini [kutofautisha] hakuna maana ya kutenganisha”. (II: 89.6-8).

- “Mafundisho ya kikatoliki hupatana na msimamo wa kiprotestanti wa kusisitiza kwamba upyaisho wa binadamu ‘hauchangii’ katika kuhesabiwa haki, wala hauwezi kamwe kuwa mchango ambao kwa njia yake mtu akate rufaa mbele ya Mungu. Hata hivyo [mafundisho ya kikatoliki] yanaona kuwa ni wajibu wake kutilia mkazo upyaisho wa mtu kwa njia ya neema yenye kuhesabia haki, ili kusudi kukiri nguvu ya Mungu yenye kuumba upya. Kwa vyovyote, upyaisho huo katika imani, matumaini na mapendo, hakika si kitu kingine isipokuwa itikio kwa neema ya Mungu isiyochunguzika.” (VII,52-53)

- “Hatuna tena sababu za kukinza, ikiwa mafundisho ya kikatoliki yanasisitiza kwamba ‘neema inahusu mtu binafsi (the personal character of grace), pamoja na inahusiana na Neno’; kwamba ‘upyaisho huu....hakika si kitu kingine isipokuwa itikio lililozalishwa na Neno lenyewe la Mungu’; na kwamba upyaisho wa binadamu ‘hauchangii katika kuhesabiwa haki wala hauwezi kamwe kuwa mchango ambao kwa njia yake mtu akate rufaa mbele ya Mungu..” (II, 89:12-21)

 

Juu ya kifungu 4.4 (aya 28-30), “Aliyehesabiwa haki kama mtu mkosefu”
(VI,102 na zifuatazo; VII,44 na zifuatazo; II,81 na zifuatazo)

- “Hao (waliohesabiwa haki) wanaanguka mara kwa mara katika dhambi zilizo zile za maisha ya kila siku, ingawa ni wenye haki na watakatifu. Zaidi ya hilo, kazi ya Roho Mtakatifu haiwatoi waamini kutoka katika mapambano ya maisha yote dhidi ya mielekeo ya kutenda dhambi. Kadiri ya mafundisho ya kikatoliki, tamaa na athari nyingine za dhambi ya asili na ya mtu binafsi zinaendelea kukaa katika waliohesabiwa haki, ambao lazima kila siku wamwombe Mungu awasamehe.” (VI,102)

- “Mafundisho yaliyotamkwa katika [Mtaguso Mkuu wa] Trento na yale ya Mababa wa Matengenezo yanapatana katika kusisitiza kwamba dhambi ya asili, na pia tamaa inayoendelea kuwepo, zinampinga Mungu... na ni kisa cha mapambano ya maisha yote dhidi ya dhambi.... [Tena, yanapatana kusisitiza kwamba] baada ya ubatizo, tamaa [iliyomo bado] katika mtu aliyehesabiwa haki, haimtenganishi tena na Mungu; yaani, kwa usemi wa Mtaguso Mkuu wa Trento, ‘si tena dhambi kadiri ya maana halisi’, na kwa usemi wa kilutheri, ‘ni dhambi iliyotawaliwa (peccatum regnatum)’”. (VII,46)

- “Suala ni kwa namna gani inawezekana kutaja dhambi kuhusu waliohesabiwa haki bila kuuwekea mipaka uhalisi wa wokovu. Kwa upande mmoja, Walutheri waeleza mvutano huu [baina ya dhambi na uhalisi wa wokovu], kwa njia ya msemo ‘dhambi iliyotawaliwa (peccatum regnatum)’ unaohusiana na fundisho la Mkristo kuwa ‘kwa wakati mmoja, mwenye kuhesabiwa haki na mwenye dhambi (simul iustus et peccator)’; kwa upande mwingine Wakatoliki wanaona kwamba haiwezekani kuhifadhi fikira ya uhalisi wa wokovu isipokuwa tu kwa kukana kwamba tamaa ina hulka ya kuwa dhambi. Kuhusu suala hili, [misimamo] imekaribiana, kiasi kwamba hati, ‘Laana za wakati...(VII)’ yataja tamaa inayoendelea kuwepo katika mtu aliyehesabiwa haki kama ‘kumpinga Mungu’, na hivyo huelekea kuwa na maana ya dhambi [kadiri ya usemi wa kilutheri]” (II,29-39)

 

Juu ya kifungu 4.5 (aya 31-33), “Sheria na Injili”

- Kufuatana na mafundisho ya Mtume Paulo, kifungu hiki kinahusu [suala la] sheria ya kiyahudi kama njia ya wokovu, ambayo imetimizwa na kudhoofishwa katika Kristo. Kauli hii na mambo yanayotokana nayo, lazima kuvielewa hivyo.

- Kuhusu kanuni 19 na 20 za Mtaguso Mkuu wa Trento, hati “Maoni ya kamati...(II:89, 28-36)” husema yafuatayo, “Ni wazi kwamba Amri Kumi zinahusu Wakristo, kama Kiri [za Kilutheri] zinavyotamka mara nyingi. Ikiwa kanuni 20 inasisitiza kwamba ‘mtu anapaswa kuzishika amri za Mungu’, hilo halileti shida kwetu; lakini ikiwa kanuni 20 inadai kwamba imani ina uwezo wa kuleta wokovu, endapo tu mtu ashike amri, hilo linatuletea shida. Kuhusu dondoo la kanuni juu ya amri za Kanisa, kama hizo ni maelezo tu ya amri za Mungu, hapana tofauti [ya msimamo] baina yetu [Walutheri na Wakatoliki]; kama sivyo, hilo linatuletea shida.”

 

Juu ya kifungu 4.6 (aya 34-36), “Uhakikisho wa wokovu”
(taz. hasa VII:59-63 na II: 90 na zifuatazo)

- “Suala ni: kwa namna gani wanadamu wana uwezo na nafasi ya kuishi mbele za Mungu licha ya udhaifu wao, na [pia] pamoja na udhaifu huo?” (VII,53)

- “Msingi na asili (vya [mafundisho ya] Mababa wa Matengenezo) ni muamana na utoshelevu wa ahadi ya Mungu na wa nguvu ya kifo na ufufuko wa Kristo; tena ni udhaifu wa wanadamu na hatari kwa imani na kwa wokovu wao itokanayo na udhaifu huo.” (VII,56)

- Pia Mtaguso Mkuu wa Trento unatilia mkazo kwamba “lazima kuamini dhambi hazisamehewi wala kamwe hazikusamehewa, isipokuwa kwa huruma ya Mungu, kwa hiari yake, kwa sababu ya Kristo”’; tena kwamba twapaswa kutokuwa na shaka juu ya “huruma ya Mungu, stahili ya Kristo, na nguvu na matokeo ya Sakramenti. Inawezekana kila mtu awe na wasiwasi na kuogopa kuhusu kuwepo kwake katika hali ya neema, anapotazama nafsi yake mwenyewe, udhaifu wake na utovu wake wa nia njema.” (Mtaguso Mkuu wa Trento, kikao cha sita, sura 9:674).

- “Luther na wafuasi wake wamepiga hatua mbele zaidi. Hao huonya kwamba si suala la kustahimili tu utovu huu wa hakika, bali inatupasa kugeuza macho yetu mbali na utovu huo wa hakika na kusadiki kibinafsi, kwa uzito na kwa namna hai, matokeo halisi ya ondoleo la dhambi linalotamkwa katika Sakramenti ya Ungamo (Kitubio), tunaloletewa ‘toka nje’. Kutokana na Yesu kusema, ‘Lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni’ (Mt 16:19), kama mwamini asingetegemea kwa hakika imara kabisa msamaha wa Mungu uliotendeka katika ondoleo la dhambi, angetaja Kristo kama mwongo.... kwa upande wa nafsi, inawezekana tegemeo hilo liwe lenye mashaka, tena ni kweli kwamba uhakikisho wa msamaha si [mtu] kudai hakika (securitas) ya msamaha; lakini mambo hayo yasiwe chanzo cha shida nyingine, yaani yampasa mwamini kugeuza macho yake mbali na hayo na kulitazama tu neno la msamaha la Kristo.”(VII,54-55)

- “Siku hizi Wakatoliki wanaweza kuthamini juhudi za Mababa wa Matengenezo za kuweka imani juu ya msingi wa ukweli halisi wa ahadi ya Kristo, “Lolote utakalolifungua duniani...”, na za kuwaelekeza waamini kwa neno maalum la ondoleo la dhambi ...Hapana sababu ya kulaani hangaiko la asili la Luther la kuwafundisha watu kukwepesha macho mbali na mang’amuzi yao, na kumtegemea Kristo tu, pamoja na neno lake la msamaha.” (V,24)

- Leo, kulaaniana kuhusu ufahamu wa uhakikisho wa wokovu, “hakuwezi tena kuwa chanzo cha kupingana, hususan tukiweka kama msingi dhana, iliyofanyika upya kuendana na Biblia, ya imani. Kwa maana inawezekana kabisa mtu apoteze au kuacha imani, tena [kuacha] kujikabidhi kwa Mungu na kwa neno lake la ahadi. Lakini, kwa vyovyote, kama akiamini, hawezi wakati huohuo kudhani kwamba Mungu si mwaminifu katika neno lake la ahadi. Kadiri ya maana hiyo, leo pia ni kweli kwamba, kwa kutumia maneno ya Luther, ‘imani ni uhakikisho wa wokovu.’” (VII,56)

- Kuhusu dhana ya imani ya Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, taz. Konstitusio ya kidogma juu ya ufunuo wa kimungu Dei Verbum, aya ya 5, “Utii wa imani...lazima apewe Mungu anapojifunua mwenyewe. Kwa imani mwanadamu hujikabidhi kikamilifu na kwa uhuru mikononi kwa Mungu, akitoa kwa Mungu mwenye kufunua ‘heshima kuu ya akili na utashi’, na akikubali kwa hiari ufunuo anaopewa na Yeye.”

- “ Hati ‘Laana za...(VII)’ haielezi wazi kwa namna ya kutosha utofautishaji wa kilutheri baina ya uhakika (certitudo) wa imani, unaomtegemea Kristo tu, na [mtu] kudai hakika ya kidunia (securitas), ambayo msingi [wa tegemeo lake] ni binadamu...Imani, kamwe haijifikirii yenyewe, bali humtegemea kabisa Mungu, ambaye neema yake inakirimiwa kwa njia ya Neno na ya Sakramenti, kwa hiyo ‘ya kutoka nje’ (extra nos)”. (II 92:2-9)

 

Juu ya kifungu 4.7 (aya 38-40) “Matendo mema ya Mtu aliyehesabiwa haki”
(taz hasa VII,66 na zifuatazo; II,90 na zifuatazo)

- “Mtaguso Mkuu [wa Trento] unakana uwezekano wa [mtu] kujipatia neema (Kan. 2; Denz. 1552) – yaani kuhesabiwa haki -; nao unaweka msingi wa kupata au kustahili uzima wa milele juu ya kipawa cha neema yenyewe, kwa njia ya kushirikishwa na Kristo (Kan. 32; Denz. 1582). Matendo mema ni ‘mastahili’ kwa sababu ni kipawa. Ingawa Mababa wa Matengenezo walilaumu ‘tegemeo kafiri’ katika matendo ya mtu mwenyewe, Mtaguso Mkuu [wa Trento] unakataa kwa dhahiri fikira yoyote isemayo kwamba mtu anaweza kudai [stahili yake]; tena, [unakataa] hakika yoyote ya uongo (sura ya 16). Ni wazi kwamba Mtaguso Mkuu [wa Trento] ulipenda kujiunganisha na Mt. Augustino, aliyeanza kutumia dhana ya ‘stahili’ kusudi kusisitiza uwajibikaji wa binadamu, ingawa matendo mema yana hulka ya kuwa kipawa [cha Mungu].” (VII,66)

- “Kama tukielewa usemi wa ‘sababu’ katika kanuni 24 [ya Mtaguso Mkuu wa Trento] kwa kutilia mkazo uhusiano [wa Mungu] na mtu binafsi, kama inavyopatikana katika sura ya 16 ya dikrii juu ya kuhesabiwa haki, inayosisitiza fikira ya ushirika na Kristo, ndipo tunapoweza kueleza mafundisho ya kikatoliki juu ya ‘stahili’ kwa jinsi yanavyotamkwa katika sentensi ya kwanza ya aya ya pili ya kifungu 4.7: kukua katika neema, kudumu katika haki tuliyopewa na Mungu na kuwa na ushirika wa kina zaidi na Kristo.

- “Sababu nyingi za kupingana zingefutika kama neno lenye tata ‘stahili’ lingefikiriwa na kuelewa kuhusiana na maana ya kweli ya neno la kibiblia ‘mshahara’ au ‘thawabu’.” (VII,67)

- “Kiri za kilutheri zinasisitiza kwamba mtu aliyehesabiwa haki ana uwajibikaji wa kutopoteza neema aliyojaliwa, tena wa kuishi katika hiyo [neema]. Kwa hiyo kiri za kilutheri zinaongelea kuhifadhi neema na kukua katika neema hiyo. Kama katika kanuni 24 [ya Mtaguso Mkuu wa Trento] haki ikifahamika kadiri ya maana ya kwamba inawaathiri wanadamu, hilo halileti shida kwetu. Lakini, kama katika kanuni 24 haki ikihusiana na Mkristo kukubaliwa na Mungu, hilo linatuletea shida, kwa maana haki hiyo ni daima kamilifu; tena, matendo ya Wakristo ni ‘matunda’ na ‘ishara’ tu, yakilinganishwa na haki hiyo.” (II,94:2-14)

- “Kuhusu kanuni 26 [ya Mtaguso Mkuu wa Trento], tutaje ‘Apolojia’ (Apoloji), inayoeleza uzima wa milele kama thawabu, ‘Twakubali kwamba uzima wa milele ni thawabu kwa sababu ni jambo linalodaiwa, [ingawa] si kutokana na stahili zetu, bali kutokana na ahadi’.” (II;94:20-22)

 

 

 

 

KIAMBATISHO CHA KAULI RASMI YA PAMOJA

1. Maelezo yafuatayo yanasisitiza maafikiano yaliyofikiwa katika Tamko la Pamoja juu ya Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki (TP), kuhusu kweli kadhaa za msingi za kuhesabiwa haki; kwa hiyo ni wazi kwamba laana za zamani za wao kwa wao hazihusu mafundisho ya kikatoliki na ya kilutheri ya kuhesabiwa haki jinsi yalivyotolewa katika Tamko la Pamoja.

2. “Kwa pamoja twakiri: Kwa neema tu, katika imani kwa tendo la wokovu la Kristo, wala si kutokana na stahili yetu yoyote, tunakubaliwa na Mungu na kupewa Roho Mtakatifu, anayefanya upya mioyo yetu na kututayarisha na kutuita kwa ajili ya matendo mema” (TP 15)

A) “Twakiri kwa pamoja kwamba Mungu husamehe dhambi kwa neema, na wakati huohuo huwaokoa binadamu na mamlaka ya dhambi yenye kuwatia utumwani (...)” (TP 22). Kuhesabiwa haki ni msamaha wa dhambi, tena ni [mtu] kufanywa mwenye haki; [tendo] ambalo kwa njia yake, Mungu “huwajalia [binadamu] kipawa cha maisha mapya katika Kristo” (TP 22). “Basi, tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu” (Rum 5:1). Twaitwa “wana wa Mungu na ndivyo tulivyo!” (1Yn 3:1). Tunafanywa upya kwa kweli na kwa ndani kwa tendo la Roho Mtakatifu, hali tukiendelea kutegemea sikuzote kazi yake ndani yetu. “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! yamekuwa mapya” (2Kor 5:17). Kadiri ya maana hiyo, Waliohesabiwa haki hawaendelei kuwa wenye dhambi.

Lakini, kama tungesema kwamba hatuna dhambi, tungekosa (Yn 1:8-10; taz. TP 28). “Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi.” (Yak 3:2). “Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri” (Zab 19:12). Tena, tunapoomba, tuseme nini, isipokuwa sawasawa na mtoza ushuru, “Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi” (Lk 18:13)? Nalo linadhihirishwa kwa namna mbalimbali katika liturujia zetu. Kwa pamoja twasikia maonyo haya, “Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake” (Rum 6:12). Hilo linatukumbusha hatari inayoendelea kuwepo, inayotokana na uwezo wa dhambi na kutenda kwake katika Wakristo. Kwa kiwango hiki, Walutheri na Wakatoliki wanaweza kumtambua Mkristo kama simul iustus et peccator (Kwa wakati mmoja mwenye haki na mwenye dhambi ); licha ya namna zao tofauti za kufikiria mada hii, kama ilivyotajwa katika TP 29-30

B) Upande wa kikatoliki na upande wa kilutheri hutumia dhana ya “tamaa” (concupiscence) kadiri ya maana [mbili] tofauti. Katika Maandishi ya Kiri za Kilutheri, “tamaa” imefahamika kama hamu ya ubinafsi ya binadamu, ambayo, kwa mwanga wa Sheria ikifahamika kiroho, inahesabiwa kama dhambi. Kadiri ya ufahamu wa kikatoliki, “tamaa” ni mwelekeo, unaodumu katika wanadamu hata baada ya ubatizo; [mwelekeo] utokao katika dhambi na kusukuma kwenye dhambi. Licha ya tofauti zilizopo hapa, kwa mtazamo wa kilutheri inawezekana kutambua kwamba hamu inaweza kuwa upenyu ambao kwa njia yake dhambi inashambulia. Kwa sababu ya uwezo wa dhambi, binadamu mzima ana uelekeo wa kumpinga Mungu. Uelekeo huo, kadiri ya dhana ya kilutheri, kama vile kadiri ya ile ya kikatoliki, “haupatani na mpango wa asili wa Mungu kwa ajili ya wanadamu” (TP 30). Dhambi inahusiana na mtu binafsi; nayo, jinsi ilivyo, inaongoza [mtu] ajitenge na Mungu. Hiyo ni hamu ya ubinafsi ya utu wa kale, na utovu wa imani na wa upendo kwa Mungu.

Uhalisi wa wokovu katika Ubatizo na hatari inayotokana na uwezo wa dhambi, vinaweza kuelezwa kwa namna ambayo kwa njia yake inawezekana, kwa upande mmoja kutilia mkazo msamaha wa dhambi na binadamu kufanywa upya kwa ubatizo katika Kristo; na kwa upande mwingine kutambua kwamba Waliohesabiwa haki nao “daima hukabiliwa na uwezo wa dhambi inayowashambulia bado (taz. Rum 6:12-14), wala hawawezi kuepukana na mapambano ya maisha yote dhidi ya kumpinga Mungu (...)” (TP 28).

C) Kuhesabiwa haki kunafanyika “kwa neema tu” (TP 15 na 16), kwa imani tu, mtu anahesabiwa haki “pasipo matendo” (Rum 3:28; taz TP 25). “Neema huumba imani, si tu imani inapoanza katika mtu, bali pia wakati wote imani inapodumu.” (Tomaso wa Aquino)[23]. Kazi ya neema ya Mungu haizuii tendo la binadamu: Mungu hutenda yote, kutaka kwetu na kutenda kwetu; kwa hiyo twaitwa kujitahidi (taz. Fil 2:12 na zifuatazo). “Ni jambo la hakika kwamba, Roho Mtakatifu akiishaanza ndani yetu kazi yake ya kuzaa upya na kufanya upya kwa njia ya Neno na Sakramenti Takatifu, mara tunaweza na tunatakiwa kushirikiana kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (...)” (Fomula ya Concordia)[24].

D) Neema, kama ushirika wao waliohesabiwa haki na Mungu katika imani, matumaini na mapendo, daima hupokelewa kutoka kwa kazi ya Mungu yenye kuokoa na yenye kuumba (Taz. TP 27). Lakini, hata hivyo, waliohesabiwa haki wanao wajibu wa kutoitumia vibaya, bali wa kuishi katika neema hiyo. Maonyo ya kufanya matendo mema ni maonyo ya kutimiza imani[25]. Matendo mema yao waliohesabiwa haki, “hao wangetakiwa kuyafanya ili kuthibitisha wito wao, yaani ili wasije wakaanguka kutoka katika wito wao kwa kutenda tena dhambi”[26]. Kadiri ya maana hiyo, Walutheri na Wakatoliki wanaweza kutambua pamoja yaliyosemwa katika TP 38 na 39 juu ya “Kuhifadhi neema”. Kwa hakika, “Yote yanayotangulia au kufuata kipawa huru cha imani katika mtu aliyehesabiwa haki, si msingi wa kuhesabiwa haki, wala hayawezi kudai kukustahili.” (TP 25).

E) Kwa njia ya kuhesabiwa haki, tunaingizwa bila masharti katika ushirika na Mungu,. ambamo imo ahadi ya uzima wa milele, “kwa maana kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika tutaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake” (Rum 6:5. Taz Yn 3:36; Rum 8:17). Katika hukumu ya mwisho, waliohesabiwa haki watahukumiwa pia kwa kadiri ya matendo yao (Taz. Mt 16:27; 25:31-46; Rum 2:16;14:12; 1Kor 3:8; 2Kor 5:10 na kadhalika). Twaelekea kwenye hukumu ambapo uamuzi wenye rehema wa Mungu utakubali mambo yote yapatanayo na mapenzi yake, katika maisha yetu na katika kutenda kwetu. Lakini, mambo yote yaliyo mabaya katika maisha yetu yatafichuliwa, wala hayataingia katika uzima wa milele. Fomula ya Concordia yasema pia, “Ni mapenzi ya Mungu na amri yake dhahiri, waamini wafanye matendo mema anayoyatenda Roho Mtakatifu ndani yao; naye Mungu anataka kupendezwa nayo kwa ajili ya Kristo, na kuahidi kuwapa thawabu yenye utukufu katika maisha haya na katika yale yajayo.”[27] Kila thawabu ni thawabu ya neema, ambayo hatuwezi kamwe kuidai.

3. Mafundisho ya kuhesabiwa haki ni kipimo au chenezo kwa ajili ya imani ya kikristo. Hapana fundisho lolote linaloweza kupinga kigezo hicho. Kwa kadiri ya maana hiyo, mafundisho ya kuhesabiwa haki “ni kigezo cha lazima kinachofaa daima ili kumwelekezea Kristo ufundishaji wote na utendaji wote wa Makanisa yetu” (TP 18). Yakiwa hivyo, [mafundisho ya kuhesabiwa haki] yana kweli yake na maana yake maalum ndani ya muktadha wa jumla wa ungamo la imani la msingi la Kanisa, lililo ungamo la Utatu Mtakatifu. Sisi [Walutheri na Wakatoliki] “twashiriki kwa pamoja lengo la kumkiri Kristo katika mambo yote, Yeye anayetakiwa kuaminiwa juu ya mambo yote kama Mpatanishi pekee (1Tim 2:5-6), ambaye kwa njia yake, Mungu, katika Roho Mtakatifu, ajitoa nafsi yake na kumimina vipawa vyake vyenye kufanya upya [vitu vyote].” (TP 18).

4. Jibu la Kanisa Katoliki halitaki kuyatilia shaka mamlaka ya Sinodi za Kilutheri, wala ya Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani. Kanisa Katoliki na Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani walianza mazungumzo na wamekuwa wakiyaendeleza kama washirika walio na haki sawa (par cum pari). Licha ya kuelewa tofauti maana ya “mamlaka katika kanisa”, kila upande haukosoi mchakato wa kuchukua maamuzi ya kimafundisho uliopangwa na upande mwingine.
 

 

 

 

KAULI RASMI YA PAMOJA
YA FUNGAMANO LA
MAKANISA YA KILUTHERI DUNIANI
NA YA KANISA KATOLIKI

1. Kwa msingi wa makubaliano yaliyofikiwa katika “Tamko la pamoja juu ya mafundisho ya kuhesabiwa haki” (TP), Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani na Kanisa Katoliki hutamka kwa pamoja kuwa, “Ufahamu wa mafundisho ya kuhesabiwa haki uliotangazwa katika tamko hili unaonyesha kwamba pana maafikiano baina ya Walutheri na Wakatoliki juu ya kweli kadhaa za msingi za mafundisho ya kuhesabiwa haki.” (TP 40). Kwa msingi wa maafikiano hayo, Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani na Kanisa Katoliki hutamka kwa pamoja kuwa, “Fundisho la Makanisa ya Kilutheri lililotolewa katika Tamko hili halipo chini ya laana za Mtaguso wa Trento. Laana zilizomo katika Kiri za Kilutheri hazihusu fundisho la Kanisa Katoliki la Kirumi lililotolewa katika Tamko hili.” (TP 41)

2. Kuhusu Azimio juu ya Tamko la pamoja la Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani lililotolewa tarehe 16 Juni 1998, na Jibu kwa ajili ya Tamko la pamoja la Kanisa Katoliki lililotolewa tarehe 25 Juni 1998, tena kuhusu masuala yaliyotokana na hati hizo mbili, kauli iliyoambatishwa (iliyoitwa “kiambatisho”), inathibitisha zaidi maafikiano yaliyofikiwa katika Tamko la pamoja. Kwa hiyo ni wazi kwamba laana za kimafundisho za wao kwa wao zilizotangulia, hazihusu fundisho la pande mbili husika kwenye mazungumzo, jinsi lilivyoelezwa katika Tamko la pamoja.

3. Pande mbili husika katika mazungumzo zinajipa sharti la kufanya utafiti endelevu na wa kina juu ya misingi ya kibiblia ya mafundisho ya kuhesabiwa haki. Tena, watajitahidi kuzidisha ufahamu wa pamoja wa mafundisho ya kuhesabiwa haki, hata zaidi ya ule uliofikiwa katika Tamko la pamoja na katika kiambatisho kinacholithibitisha. Kwa msingi wa maafikiano yaliyofikiwa, mazungumzo endelevu yanatakiwa, hasa kuhusu mada zilizotajwa kwa namna maalum katika Tamko la pamoja lenyewe (TP 43) kama zile zinazohitaji ubainifu zaidi ili kupata kufikia ushirika kamili wa kikanisa, na umoja katika utofauti, ambamo hitilafu zinazobaki “zipatanishwe”, zisiwe na uwezo tena wa kusababisha matengano.

Walutheri na Wakatoliki wataendelea kujitahidi kwa roho ya kiekumeni katika ushuhuda wao wa pamoja, ili kufafanua ujumbe wa kuhesabiwa haki kwa njia ya usemi wenye kuwagusa watu wa sasa, na kwa kuuhusisha na mahangaiko ya mtu binafsi na ya jamii ya wakati wetu huu.

Kwa kutia saini hati hii, Kanisa Katoliki na Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani huthibitisha “Tamko la pamoja juu ya mafundisho ya kuhesabiwa hakikatika uzima wake wote.

 

 

 

 

[1] The Smalcald Articles, II,1; Book of Concord, 292.

[2] “Rector et yudex super omnia genera doctrinarum”, Weimar Edition of Luther’s Works, 39, I, 205

[3] Inafaa kusisitiza kwamba baadhi ya Makanisa ya Kilutheri, Kiri zake za lazima kufuatwa ni mbili tu, yaani Ukiri wa Ausburg na Katekismo Ndogo ya Dk Martin Luther. Katika Maandishi hayo hapana laana yoyote juu ya Kanisa Katoliki la Kiroma kuhusu [mafundisho ya] kuhesabiwa haki.

[4] Ripoti iliyotolewa na Tume ya Pamoja ya Kilutheri-Kikatoliki; taz. “Growth in agreement” (New York; Geneva 1984; 188-189).

[5] Ripoti iliyochapishwa na Fungamano la Makanisa ya Kilutheri duniani (Geneva, 1994).

[6] “Lutheran and Catholics in Dialogue”, VII (Minneapolis 1985).

[7] Minneapolis, 1990.

[8] Taz. “Okumenische Rundschau” 44 (1995): 99-102.

[9] Neno “Kanisa” limetumika katika Tamko hili kadiri linavyoeleweka na Makanisa husika, bila kufikiri kutatua masuala ya eklesiolojia yanayohusiana na neno hilo.

[10] Taz. “Ripoti ya Malta”, 26-30; na ripoti “Kuhesabiwa haki kwa imani”; 122-147

[11] Dogma ni fundisho kuu au kanuni ya imani ya sharti

[12] “Wote chini ya Kristo mmoja”, 14; Katika “Growth in Agreement”, 241-247

[13] Weimar Edition of Luther’s Works, 8, 106

[14] Taz. H. Denzinger,”Enchiridion Symbolorum, definitionum et declarationum de rebus fidei et morum”, 1528

[15] Taz Denz., 1530

[16] Cf. Apology II:38-45; Book of Concord, 105f.

[17] Taz. Denz, 1515

[18] Taz. Denz., 1515

[19] Taz. Denz., 1545

[20] Taz. Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusio ya kidogma juu ya ufunuo wa kimungu Dei Verbum, 5

[21] Taz. Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusio ya kidogma juu ya ufunuo wa kimungu Dei Verbum, 4

[22] Taz ripoti “Laana za kimafundisho…”, 32

[23] S. Th. II/II 4, 4 ad 3.

[24] FC SD II, 64f: BSLK 897,37ff.

[25] Taz. BSLK 197,45

[26] Apol. XX,13, BSLK 316,18-24; kuhusu 2Pet 1:10. Taz. pia FC SD IV,33; BSLK 948,9-23

[27] FC SD IV, 38